MICHAEL MTANZANIA

ONESTEPMEDIATZ

Kagera inaweza kuifunga Simba ikiwa Mexime, Mbaraka Yusuph, hawatokuwa na kikomo…


WAKATI ushindi wa aina yoyote dhidi ya Azam FC  leo Jumamosi utawapeleka mabingwa watetezi Yanga SC katika kilele cha msimasmo wa ligi kuu Tanzania Bara, Simba SC kesho Jumapili watakuwa uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika kibarua kigumu watakapowavaa wenyeji Kagera Sugar FC.

Kagera iliyo katika nafasi ya nne na alama 42 baada ya kucheza michezo 24
ilitolewa katika michuano ya FA Cup baada ya kuchapwa 2-1 na Mbao FC katika mchezo war obo fainali uliopigwa katika uwanja huo wa Kaitaba wiki iliyopita.

MBARAKA YUSUPH

Kocha Mecky Mexime anajivunia ‘utitiri’ wa washambuliaji katika kikosi chake, lakini ataendelea kumtegemea mfungaji wake namba moja kijana Mbaraka Yusuph ambaye tayari amefunga magoli kumi hadi sasa katika VPL.

Ame Ally alifunga goli lake la kwanza akiichezea Kagera katika kichapo dhidi ya Mbao na huenda mshambulizi huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Azam FC na Simba akaanza katika safu ya mashambulizi sambamba na Yusuph ambaye alifunga goli lake la kwanza la kimataifa katika mchezo wake wa kwanza akiichezea Taifa Stars Jumanne iliyopita.

Danny Mrwanda, Ibrahim Twaha, Themi Felix, Edward Christopher na Paul Ngwai wote hawa ni washambuliaji ambao wanaweza kuibeba Kagera ikitokea wakapata nafasi katika mchezo wa kesho.

Kagera hutafuta bao kwa nguvu zote wanapocheza nyumbani, hucheza mchezo wa kuvamia lango la wapinzani wao ndiyo maana licha ya kuchapwa 6-2 na Yanga katika mchezo wa raundi ya kwanza katika uwanja huo lakini bado walionekana kucheza kwa kushambulia muda wote wa mchezo.

Yusuph atawasaidia sana katika mchezo dhidi ya Simba, anachotakiwa kufanya ni kutokuwa na ukomo wa kufanya vizuri, na kama ataendelea kucheza kwa umakini uleule uliomfikisha hapo alipo anaweza kufanya kitu kinachoweza kumng’arisha zaidi. Yusuph anapaswa kuongeza bidii zaidi na hilo litasaidia kuifunga timu yake ya zamani ambayo alikataa kujisajili nayo msimu huu.

Kagera wamefanikiwa kufunga magoli 26 na kuruhusu magoli 21. Si wastani mzuri sana katika kuzuia lakini bado wanaweza kumtegemea kipa mzoefu Juma Kaseja na safu ya walinzi wazoefu kama Mohamed Fakhi, Anthony Matogolo na George Kavila ili kuhakikisha Simba wanaangusha pointi.

LAUDIT MAVUGO, IBRAHIM AJIB

Inaonekana kocha wa Simba, Joseph Omog amekwisha pata safu yake ya mashambulizi. Katika michezo ya karibuni amekuwa akiwapanga washambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo na kijana Ibrahim Ajib. Wawili hao wamefanikiwa kufunga magoli kumi kati ya 40 ambayo timu yao imefanikiwa kufunga hadi sasa katika ligi.

Ili Shiza Kichuya aanze ni lazima Juma Ndanda Liuzio aanzie benchi. Wakati Fulani mwanzoni mwa michezo ya mzunguko wa pili Omog alikuwa akiwapanga washambuliaji wake watatu-Liuzio, Mavugo na Ajib lakini hakukuwa na matokeo mazuri upande wao. Timu ilionekana kushindwa kufunga magoli na hata kukosa ‘balansi’ katika eneo la kiungo.

Lakini baada ya kuwarudisha kikosi cha kwanza Kichuya na Said Ndemla angalau unaweza kuona uhai katika safu ya ufungaji ndiyo maana hata yule ‘aliyekuwa hafungi-Mavugo’ ameanza kufanya hivyo kwa sababu amekuwa akipasiwa pasi nyingi anazozitaka.

BEKI YA SIMBA

Pamoja na mabadiliko yote hayo bado hakuna kazi rahisi dhidi ya Kagera na licha ya kuruhusu magoli kumi bado wanaweza kujikuta wakiadhibiwa na Kagera ambao pia wana kikosi kizuri na kocha bora nchini.

Kumkosa Method Mwanjale katika michezo ya karibuni kulionekana kuathiri uwezo wa beki ya Simba lakini sasa amerejea Mganda, Juuko Murishid ambaye atacheza sambamba na Abdi Banda katika safu ya ulinzi wa kati.

Wawili hao wanaweza kukutana na wakati mgumu mbele ya Yusuph, Ame, Themi, Mrwanda ambao wana kasi na uwezo wa kumiliki mpira. Ili kupata kikosi kilichobalansi nguvu, ufundi na mbinu ingekuwa vizuri kwa kocha Mecky kutumia mfumo wa 4-3-3 ambao utawaruhusu kushambulia zaidi.
Kwa aina ya walinzi wa pembeni wa Simba (Besala Bokungu-beki namba mbili na Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr-beki ya kushoto) Kagera haitakuwa na wakati mzuri wakitumia mfumo wa 4-4-2 kwa maana hawana wing walio fiti ambao watawafanya Bokungu na Zimbwe Jr kutoshambulia mara kwa mara.

Ili kuiweka hatarini beki ya Simba, Mecky angewapa nafasi ya kuanza mchezo Mrwanda, Yusuph na Themi  kama wachezaji hao wapo fit. Kucheza kwao watatu kutawafanya walinzi wa Simba kutoshambulia sana na hilo litaisaidia Kagera ambao hawana-cha kupoteza hadi sasa.

MUZAMIRU, NDEMLA, KOTEI, KICHUYA

Omog anaweza kuwaanzisha viungo hawa wane katika mfumo wa 4-4-2 ambao umekuwa ukimpatia magoli. Ili kuuvuruga mfumo huu Mecky atahitasji wachezaji wake kumiliki sana mpira na kupitia katikati ya uwanja ambako si rahisi ila ni salama zaidi kwao kwa sababu Simba inategemea kasi ya Zimbwe Jr kupeleka mashambulizi wakipitia upande wao wa kushoto na Shiza Kichuya katika upande wa kulia.

Naamini uwepo wa viungo watatu katikati ya uwanja upande wa Kagera utamfanya Ndemla kutopiga pasi zake za hatari mara kwa mara na watapunguza nafasi ya Muzamiru kusogea zaidi hadi katika eneo lao la hatari na kuwatengenezea nafasi washambuliaji wake au kufunga yeye mwenyewe.

Simba wana viungo wazuri katika makaratasi lakini hilo si jambo litakalowafanya watawale mchezo. Walisumbuliwa sana katikati ya uwanja na timu ya daraja la chini Madini FC katika robo fainali ya FA Cup, hivyo Kagera wanaweza kutumia nafasi ya kucheza nyumbani na uzoefu wa wachezaji wake kushinda mechi hii.

Takwimu za Kagera Sugar vs Simba katika mechi saba zililizopita za ligi kuu Tanzania bara

02/04/2017 Kagera Sugar ?? Simba
15/10/2016 Simba 2-0 Kagera Sugar
07/02/2016 Kagera Sugar 0-1 Simba
20/09/2015 Simba 3-1 Kagera Sugar
06/04/2015 Kagera Sugar 1-2 Simba
26/12/2014 Simba 0-1 Kagera Sugar
05/04/2014 Kagera Sugar 1-1 Simba
31/10/2013 Simba 1-1 Kagera Sugar

Takwimu za Kagera na Simba katika msimu huu 2016/17 

Simba mechi 24 – Kagera mechi 24
Ushindi: Kagera Sugar 12 – Simba 17
Sare: Kagera Sugar 6 – Simba 4
Walizopoteza: Kagera Sugar 6 – Simba 3
Magoli ya kufunga: Kagera Sugar 26 – Simba 40
Magoli ya kufungwa: Kagera Sugar 21 – Simba 10
Mechi bila kuruhusu goli: 14 – Simba 16
Points: Kagera Sugar 42 – Simba 55
Nafasi: Kagera Sugar 4 – Simba 1

Post a Comment

0 Comments