Chama cha Soka Visiwani Zanzibar “ZFA” kimesimamisha kutoa zawadi ya mpira kwa mchezaji yeyote ambae atafunga mabao 3 (Hat-trick) kwenye mchezo dhidi ya timu ya Kimbunga ambayo ndiyo inayoburura mkia katika ligi kuu soka Visiwani Zanzibar.
Akithibitisha taarifa hiyo Afisa habari wa ZFA Ali Bakar ‘Cheupe’ amesema ni kweli wamesitisha kutoa zawadi ya mpira kwa mchezaji wa timu yoyote ambayo itakayocheza dhidi ya Kimbunga.
“Ni kweli tumesitisha kutoa zawadi hiyo, kamati ya ligi ambayo inayoongozwa na Makamu wa Rais ZFA Unguja Mzee Zam Ali imekaa pamoja na kuona kwamba timu ya Kimbunga inakuja kucheza bila ya kuwa na ushindani, sasa kwa mchezaji yeyote ambae atakaepiga Hat-trick dhidi ya timu hii hatopatiwa tena mpira, na jambo hili si kama kanuni tena wala haimo katika katiba ata iwe ni lazima kutoa zawadi hiyo tuliweka kama ni heshma tu, hivyo kuanzia michezo inayofuata ya Kimbunga zawadi hiyo haitotolewa tena, hayo ndio maamuzi ya kamati baada ya kukutana,” alisema Cheupe.
Nae katibu wa timu ya Kilimani City Ramadhan Juma amesikitishwa kwa hatua hiyo waliyoichukua ZFA kwa kusema kuwa si jambo zuri na watapunguza hamasa kwa wachezaji.
“Kwa hili mimi siliungi mkono hata kidogo na sijuwi kama ZFA wanaielewa vizuri Hat-trick, hii ni zawadi ya mchezaji aliyefanya tendo hilo la kufunga mabao matatu na sio kwa timu iliyofungwa matatu, sasa hili jambo litapunguza hamasa kwa vijana wetu, tumeshuhudia Arsenal hata wakicheza na timu ya daraja la pili mchezaji akipiga Hat-trick anapatiwa zawadi yake kwaiyo ubovu wa Kimbunga sioni sababu ya kutotowa zawadi hiyo, na kama zawadi hawana waseme tu, na wakitoa maamuzi kama hayo bora wakae na watu wa mpira ili kujadiliana nini kifanyike, kwa hili ZFA wamechemka sana hapa”. Alisema Ramadhan
.
Kimbunga ndiyo timu inayokamata nafasi ya mwisho (18) katika ligi kuu soka ya Zanzibar Kanda ya Unguja ambapo imeshafungwa jumla ya mabao 96 katika michezo 27 waliyocheza na kwasasa zaidi ya Hat-trick 10 zimeshafungwa katika ligi huku wachezaji wengi wakipiga Hat-trick wanapokutana na timu hiyo ambayo tayari imeshaonja kipigo cha mabao 10-0, 8-0, 7-0 na bado kuna baadhi ya vilabu wakipania kupata ushindi kuliko huo.
0 Comments