Klabu ya Yanga atakosa huduma ya mshambuliaji wake Mzimbabwe, Donald Ngoma, baada ya mchezaji huyo kurudishwa hospitali kwa ajili ya kuendelea na matibabu ya goti ambayo yanamsumbua kwa muda mrefu.
Daktari wa timu ya Yanga Edward Bavu, ameuambia mtandao wa Goal, Ngoma hali yake imezidi kuwa mbaya baada ya kujitonesha goti hilo Jumamosi kwenye mchezo dhidi ya Zanaco.
“Nimemshauri kocha kumuondoa kwenye orodha ya wachezaji watakao kwenda Zambia kwa ajili ya mchezo wa marudiano kwasababu hali yake siyo nzuri na nimelazimika kumuanzishia matibabu upya,”amesema Bavu.
Daktari huyo amesema kwa namna alivyogundua ukubwa wa tatizo hilo, anafikiria mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima uliobakia na anaweza kuwa tayari hadi mwanzoni mwa msimu ujao wa ligi ya Vodacom.
Amesema awali walidhani tatizo hilo litakuwa dogo lakini baada ya kuliangalia kwa undani wamebaini kuwa ni tatizo kubwa ambalo linahitaji kupata tiba maalumu ili aweze kupona na kurejea kwenye majukumu yake ya kuipigania Yanga.
Ngoma kabla ya taarifa hizo alirejea uwanjani katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Jumamosi lakini hakuweza kumaliza mchezo na kutolewa kipindi cha pili.
Kikosi cha Yanga kinaondoka Alhamisi kuelekea Zambia kwa ajili ya pambano hilo la marudiano na Zanaco na hadi sasa hakuna matumaini ya nyota huyo muhimu kutoka Zambia kuwa anaweza kutoa mchango wake.
0 Comments