Uongozi wa klabu ya Yanga kupitia Msemaji wake, Dismas Ten, umepuuzia taarifa zilizoenea mitandaoni na katika baadhi ya vyombo vya habari zikieleza kuwa mapato ya fedha yaliyotokana na uuzaji wa kalenda na majarida yake zimeishia mifukoni mwa baadhi ya viongozi.
Ten ameeleza hayo akisema kuna baadhi ya watu waliokuwa viongozi wa Yanga wameamua kuanzisha kampeni ya chini kwa chini ili kuichafua klabu hiyo iliyopo mitaa ya Twiga, Jangwani.
Msemaji huyo amesema watu hao wamekuwa wakiichafua Yanga wakihitaji kurejea kwa ajili ya kuitumikia klabu japo imekuwa si rahisi kutokana na kukosa nafasi katika utawala uliopo hivi sasa.
Kufuatia taarifa hizo, Ten ameeleza kuwa hazina ukweli wowote na akiomba wadau wote wa Yanga kuzipuuza sababu hazina malengo chanya na uongozi uliopo pamoja na klabu kwa ujumla.
Taarifa hizi zimeanza kuja ikiwa Yanga imeanza mchakato wa kuelekea uchaguzi wa kumpata Mwenyekiti wa klabu baada ya kukaa muda mrefu bila ya kuwa naye.
0 Comments