Siku chache baada ya kuibuka hofu kuwapo kwa uwezekano wa Shirika la
Umeme nchini (Tanesco) kuikatia nishati hiyo Zanzibar kutokana na deni
inalodaiwa, visiwa hivyo vimepata matumaini ya kuwa na umeme wake wa
uhakika.
Matumaini ya Zanzibar kuondokana na tatizo la umeme wa kutegemea sehemu
moja yameanza kuonekana baada ya utafiti wa nishati mbadala
unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kuonyesha uwezekano wa rasilimali
hiyo kupatikana bila ya matatizo visiwani hapa.
Akizungumza katika ziara iliyofanyika jana kwenye vituo vya utafiti wa
uzalishaji umeme wa upepo na nishati ya jua mikoa ya Zanzibar, Meneja wa
mradi huo, Munir Shirazi Hassan alisema utafiti ulioanza mwaka 2016 kwa
ufadhili wa EU unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na
kufuatiwa na ushauri yakinifu kutoka kwa wataalamu.
“Tunasubiri kwa hamu huduma hii ianze kutumika, tunadhani kufanikiwa
kwake kutasaidia kushuka kiwango cha matumizi ya umeme kutoka Tanesco
kwa zaidi ya asilimia 50 ili kuondokana na deni la matumizi ya kila
mwezi.”
Ofisa mawasiliano kutoka Kampuni ya Ubelgiji, Sebastian Sanga alisema
kukamilika kwa mradi huo kutaiondolea Zanzibar adha ya kutegemea umeme
kutoka sehemu moja.
0 Comments