Na Mohamed Mansour Nassor
Mashindano ya Kombe la dunia la watoto wa mitaani chini ya shirika la Steet Child United na udhaamini wa makampuni tofauti na taasisi tofauti lakini zaidi kampuni ya mawasiliano ya simu ya nchini Urusi, Megafon yamefikia tamati leo kwa kuchezwa mechi za mshindi wa tatu na fainali kwa wanawake na kwa wanaume.
Mshindi wa tatu kwa wanawake ni Uingereza baada ya kuifunga Ufilipino magoli 2-0 na kwa wanaume ni Burundi baada ya kuibwaga Indonezia magoli 3-1. Fainali kwa wanawake ilikua Tanzania na Brazil na Brazil iliifunga Tanzania 1-0.
Goli hilo lilifungwa Mwisho wa kipindi cha kwanza baada ya kutokea mawasiliano mabaya kati ya mlinzi wa Tanzania na mlinda mlango wake. Mchezo huo pia ulikua ni wa aina yake na wa wa kasi sana na wa kutafuta kosa na timu mojawapo na kuiadhibu timu nyengine kwa kosa hilo.
Tanzania ilikua na nafasi za kufunga kipindi cha kwanza lakini ilikua haifanyi vizuri katika umaliziaji. Brazil walimiliki mchezo sana na hasa viungo wao walimficha kiungo mkuu wa Tanzania, Nahodha Asteria Robert na hapo Tanzania ikawa ishadhibitiwa.
Kipindi cha pili Tanzania kidogo walicheza vizuri lakini hawakurudisha goli hilo. Kipindi cha kwanza Tanzania walicheza kwa presha sana na hawakutulia na mpira na hali hio ikawapotezea kujiamini. Lakini mwisho wa siku asiekubali kushidwa sio mshindani. Tanzania tukashika nafasi ya pili katika mashindano hayo kwa wanawake.
Kwa upande mwengine mechi hio ya fainali ilihudhuriwa na watu wengi mashuhuri na mahususi na viongozi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi. Wageni hao ni mmoja wapo ni mchezaji wa zamani wa Arsenal na bingwa wa kombe la dunia kwa kikosi cha Brazil na kiungo maarufu na mwenye uwezo wa viwango vya dunia, Gilberto Da Silva.
Kiungo huyu ameichezea Brazil na ameshinda kombe la dunia mwaka 2012 na ameshinda kombe la ligi kuu ya Uingereza na Arsenal na pia alicheza klabu ya Olimpiakos ya Ugiriki na pia alishawahi kushinda kombe la Copa America na Brazil na kombe la klabu bingwa barani America ya kusini au Copa Liberatadores.
Timu zote baada ya mechi zilipata nafasi ya kumuuliza swali moja Gilberto Da Silva. Tanzania iliuliza swali kupitia Nahodha wake, Asteria Robert kwa Kiswahili na mkalimani Mohamed Masour Nassor akatafsiri moja kwa moja kwa lugha ya Kireno ya mchezaji huyo. Swali hilo lilikua hivi,"Je ni vipi Unawasaidia watoto wa mitaani kufikia ndoto zao na wale watoto ambao wanataka kuwa wachezaji wa viwango vya dunia kama wewe?
Mwisho ikafuata sherehe ya ufungaji wa mashindano hayo. Wageni mashuhuri wengi walikuako wakiwemo Rais wa chama cha Mpira wa Urusi, Mkurugenzi mkuu wa kampuni iliodhamini ya Megafon na shirika la Street Child United kutoka Uingereza.
Mabalozi Mbalimbali wakiwepo mabalozi wa kombe la dunia la FIFA la 2018 nchini Urusi, Mkurugenzi wa masuala ya jamoi na utamaduni wa chuo cha Patrice Lumumba, wachezaji wa zamani wa Urusi,Mchezaji Gilberto Da Silva, Mwaandishi Mkubwa wa gazeti la michezo la Urusi kutoka mji wa Saint Petersburg na wengine.
Muda wa zawadi ulipofika, Tanzania ilizawadiwa Kombe na medali za shaba kwa kila mchezaji na viongozi wa timu kutoka chama cha mpira cha Urusi na zawadi zengine kutoka kwa chuo cha Patrice Lumumba. Tanzania pia ilitoa kiungo bora wa mashindano ambae ni nahodha, Asteria Robert ambae kwa kweli alistahili sana.
Kwa upande wa bingwa wa wanaume ni Timu ya Uzbekistan baada ya kuilaza kwa mikwaju ya penati timu ya Pakistan. Kwa upande wa zawadi zengine, Mlinda Mlango bora alitoka Uingereza kwa wanawake, kwa wanaume alitoka Indonezia, Mfungaji bora kwa wanawake alitoka Brazil, mlinzi bora kwa wanawake alitoka Ufilipino, mlinzi bora kwa wanaume alitoka Uzbekistan, mchezaji bora kwa wanaume alitoka Pakistan, mchezaji bora kwa wanawake alitoka Brazil na wengine.
Mashindano hayo yamefikia tamati huku yakiwa yameleta faida kubwa sana katika mpira kama mashindano lakini pia kujuana kwa watoto hawa wa dunia nzima na pia kufanya utalii sehemu mbalimbali za mjia wa Moscow na kujifunza kwa mambo mengi sana ikiwepo kufanya mikutano au congress za watoto hawa na kujifunza ujuzi kutoka nchini mbalimbali pamoja na watoto kupewa nafasi ya kusema mawazo yao na changamoto zao na kuahidiwa kusaidia. Nchi zilizoshiriki ni 21 na timu zikiwa ni 24.
Tanzania kwa ujumla imeweka rikodi nzuri pia kwa kuwa mshindi wa pili mwaka huu kwa wanawake. Mwaka 2014 Tanzania ilikua bingwa wa mashindano haya kwa wanaume huko mjini Rio di Jeneiro, Brazil na mwaka 2010 Tanzania iliishia nusu fainali huko Afrika ya Kusini kwa upande wa wanaume. Nafikiri mwaka 2022 nchini Qatar, Tanzania kwa wanawake itafanya vizuri zaidi. Ahsante sana.
0 Comments