MICHAEL MTANZANIA

ONESTEPMEDIATZ

Jicho la 3: ‘Ni lazima Lwandamina ashinde vs Azam FC vinginevyo atakuwa si kocha sahihi Yanga’




NI ALAMA za nyakati ambazo kocha George Lwandamina anatakiwa kuzisoma kuhusu ubora wa wachezaji wake.

Baadhi ya watu wanasema nyota wengi wa kikosi cha Yanga SC umri ‘umewatupa’ lakini wanasahau kuwa ni
kikosi hikihiki kinacho-pepesuka chini ya Lwandamina ndicho kilichoshinda mataji mawili ndani ya Tanzania na kufika hatua ya 16 bora katika ligi ya mabingwa Afrika kisha kufuzu kwa hatua ya makundi katika Caf Confederation Cup msimu uliopita chini ya Mholland, Hans van der Pluijm.

Lwandamina hatakwepa lawama ikiwa Yanga itashindwa kutetea ubingwa wake wa ligi kuu, FA Cup na kushindwa kuifikisha timu hiyo katika hatua ya makundi ya Confederation Cup walipoangukia baada ya kutolewa hatua ya 32 bora katika ligi ya mabingwa na timu isiyo na uzoefu-Zanaco FC katikati ya mwezi huu.

Kuelekea mchezo wa Jumamosi hii kati ya Azam FC vs Yanga, Lwandamina anapaswa kusimama kama kiongozi mkuu wa vita huku akitambua kushindwa kupata ushindi kwa namna yoyote ni pigo katika mbio za ubingwa.

POINTI 18 ZA ‘KUFA NA KUPONA’

Ikiwa imesalia michezo 6 kabla ya kumalizika kwa msimu-inamaana kila timu ina pointi 18  muhimu za kuisaidia kutimiza malengo yao, Yanga wako nyuma kwa alama mbili zaidi dhidi ya mahasimu wao Simba SC ambao watakuwa Katiba Stadium kucheza na Kagera Sugar siku ya Jumapili.

Ushindi dhidi ya Azam FC kesho utaipeleka Yanga kileleni kwa alama moja zaidi, na hilo litapeleka presha kwa Simba kuhakikisha wanaishinda Kagera Sugar ili kuwaengua Yanga kileleni siku ya Jumapili.

Yanga hawapaswi kujilaumu kwa kushindwa kuifunga Mtibwa Sugar wiki tatu zilizopita na kukwea kileleni baada ya Simba kuangusha pointi mbili katika uwanja wa Taifa walipocheza na Mbeya City FC siku moja kabla ya Mtibwa v Yanga.

Bali wanapaswa kuchukulia matokeo ya kupoteza mkwaju wa penati kwa winger Saimon Msuva katika suluhu-tasa vs Mtibwa kama funzo litakalowaongezea umakini na nidhamu ya mchezo katika mchezo mgumu zaidi watakapocheza dhidi ya Azam FC wikendi hii.

Katika historia yao VPL, Azam FC pekee ‘inayoisumbua zaidi’ Yanga, na mabingwa hao wa kihistoria wa Bara hawawezi kupinga hilo kwa maana katika mipambano yao 17 iliyopita katika VPL kila timu imefanikiwa kupata ushindi katika michezo mitano huku michezo 7 ilimalizika kwa sare.

AZAM FC WANACHEZA KITIMU ZAIDI TOFAUTI NA YANGA

Azam FC huenda wana kikosi kipya zaidi ya Yanga na licha ya kutokuwa na msimu mzuri katika ligi na kuondolewa raundi ya kwanza katika Caf Confederation Cup lakini bado Azam FC inacheza kitimu hasa katika mipambano mikubwa.

Wachezaji wazoefu kikosini kama Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, David Mwantika na Aggrey Moris katika safu ya ulinzi wameweza kuwapokea vizuri nyota wa kulipwa kama Mzimbabwe, Bruce Kangwa na raia wa Cameroon, Yakub Mohamed ambao wameingia msimu huu na kufanya vizuri.

YANGA WANAPASWA KUCHEZA KITIMU  

Wachezaji wa Yanga wanapaswa kucheza kitimu, walikuwa wakicheza hivyo huku wakiajiamini chini ya Hans lakini ndani ya miezi mitatu chini ya Mzambia, Lwandamina si wale walioshinda mataji ya VPL na FA msimu uliopita.

Wamepunguza hamasa yao ya kusaka na kulazimisha matokeo, na sasa wanapaswa kujituma zaidi ili kushinda ubingwa wa tatu mfululizo. Kwa namna walivyocheza hadi kufika walipo sasa, wanaweza kutimiza matarajio yao.

Kufunga magoli 49 katika michezo 24 hakuwezi kuwapa matarajio makubwa mbele ya Azam FC ambao wameruhusu nyavu zao mara 15 na kufunga magoli 29 tu katika game 24 walizokwisha cheza.
Endapo Donald Ngoma atarejea uwanjani kwenye mechi ya kesho ni habari njema zaidi kwa kikosi cha Lwandamina, hata kama atamkosa Amis Tambwe bado kocha huyo anaweza kuwapanga Ngoma, Msuva na Mzambia, Obrey Chirwa kama washambuliaji watatu katika mfumo wa 4-3-3.

MAHUNDI, SINGANO vs KESSY, MWINYI NI TATIZO

Beki ya Azam imekuwa ikiimarika tangu kuanza kwa mzunguko wa pili lakini inaweza kupitika ikiwa timu pinzani itashambulia kwa kasi. Ugumu ambao unamkabili Lwandamina ni namna gani safu yake ya ulinzi itaweza kuendana na kasi ya viungo wa pembeni wa Azam FC, Joseph Mahundi na Ramadhani Singano ambao watacheza kumzunguka Mghana, Yahya Mohamed.

Si shaka kuhusu uwezo wa Rambdhani Kessy ambaye alipata umaarueu mkubwa nchini Novemba, 2014 baada ya kumzima Singano katika mchezo uliowakutanisha wakiwa timu za Mtibwa (Kessy) na Simba (Singano).

Lakini wasiwasi ni lazima utakuwepo kuhusu mbinu za kujilinda za Mwinyi Hajji  katika  beki namba tatu, hasa  akicheza  dhidi  ya Mahundi mwenye  kasi,nguvu  na  uwezo  wa kukimbia  na  mpira. Hajji  amekuwa  akipoteza mipira  mara  kwa  mara  na  mbaya  zaidi  amekuwa akipoteza mipira  hiyo  akiwa  katika  eneo  lake  la  ulinzi.

HIMID, DOMAYO, SALUM vs NIYONZIMA, ZULU, KAMUSOKO

Mechi  hii  inaweza  kuamuliwa  zaidi  na  namna  safu  za  viungo   zitakavyocheza. Azam FC wamekuwa  wakiwatumia Himid Mao, Salum Abubakary  na Frank Domayo  katikati ya uwanja na watatu hao katika ligi ya Bara wamekuwa wakitawala mechi.

Ili kujaribu kuizuia Azam FC katikati ya uwanja kocha Lwandamina  anaweza kuwapanga Mzambia, Justine Zulu katika eneo la kiungo wa ulinzi, Mzimbabwe ,Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima  wakiichezesha  timu. Hawa ni viungo watatu wa Kimataifa na Yanga inawahitaji kuonyesha uwezo wao  sasa ili timu inufaike.

Kucheza hawa watatu  inasaidia  kwa maana  watakuwa  na mtazamo  mpana wa kulinda na kushambulia, lakini  haitawarahisishia  kwa maana Himid, Domayo na Salum ni wagumu  na wana ustahimilivu mkubwa ndani ya uwanja.

Azam hupasiana pasi fupifupi za uhakika na mara chache  Domayo  amekuwa  akipiga pasi  ndefu za uhakika ili kutawala mechi Yanga italazimika kupeleka mipira mirefu pembeni ya uwanja ambako Zulu  na Msuva  watakuwawepo.

AZAM FC BILA BOCCO

Ni faida kubwa kwa Yanga kwa maana kutokuwepo kwa ‘kiboko’ yao nahodha John Bocco  huenda wasikutane  na makali zaidi  ikiwa angekuwepo. Vicent Bossou na Nadir Haroub inaweza kuwa beki sahihi ya kucheza dhidi ya Yahya katika safu ya kati.

Azam wamekuwa wakikabiliwa na tatizo katika ufungaji na kitendo cha kumkosa Bocco  aliyefunga magoli nane kati ya 29 waliyofunga katikaligi ni tatizo ambalo linaweza kuwaangusha zaidi. Wanaweza kutegemea mashuti ya mbali kutoka kwa Domayo, Salum,Mahundi na Himid na kama  ikitokea wakatangulia kupata goli itakuwa rahisi kwao  kupata matokeo.

Ni lazima Lwandamina ashinde vs Azam FC vinginevyo  atakuwa si kocha sahihi Yanga hasa ukizingatia tayari ameshindwa kuifunga Simba katika michezo miwili, ameshindwa kuifunga timu ya kawaida Zanaco FC, amepoteza 4-0 mbele ya Azam FC na ameshindwa kuzifunga timu kama Mtibwa, African Lyon katika nyakati ambazo timu ilipaswa kuchukua pointi.

Post a Comment

0 Comments