MICHAEL MTANZANIA

ONESTEPMEDIATZ

Waomba JPM aondoe katazo la pombe ya viroba




UMOJA wa Wafanyabiashara wa vileo katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, wamemwomba Rais John Magufuli kuingilia kati na kusitisha zuio la pombe kali inayofungwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba).

Pia wamemuomba awaongezee miezi sita zaidi ili wamalize kuuza shehena iliyopo kwenye maghala yao.

Mwenyekiti wa umoja huo , Renatus Mlelwa, alisema kuwa zuio hilo limekuwa la ghafla ambapo wengi wao walikuwa tayari wamenunua shehena ya kutosha tangu Desemba mwaka jana, hivyo wamepata hasara kubwa huku taasisi za kifedha ambazo zimewakopesha zikiwasumbua.

“Tunamwomba Rais wetu aingilie kati zuio la uuzaji wa pombe iliyofungwa kwenye vifungashio vya plastiki maarufu viroba. Alisimamishe na tunamuomba atupatie miezi sita zaidi ili tuweze kuuza shehena tuliyonayo maghalani, kwa kuwa ni bidhaa ya mikopo tuliyokopeshwa na taasisi za kifedha ambapo sasa tumeingia migogoro nayo “ alisema.

Kwa upande wake, Dando Samson ambaye ni mwanachama wa umoja huo alisema kuwa licha ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na uuzaji na uuzwaji wa kiel hicho bado wanamwoba Rais Magufuli awaonee huruma kwa kuwaongezea miezi sita zaidi ili wamalize shehena waliyonayo.

“Kufungwa kwa viwanda vinavyotengeneza kileo hicho hatuna tatizo na agizo hilo lakini kwa upande wetu Rais (Magufuli ) atuonee huruma asitishe zuio hilo na atuongezee miezi sita zaidi ili tumalize stock tuliyonayo,“ alisisitiza.

Naye Julio Myovela aliyejitambulisha kuwa ni Wakala wa Tanzania Breweries Limited (TBL) na Tanzania Distillers Limited td (TDL) aliitaka Serikali iwaangalie upya kuhusuiana na zuio hilo kwa kuwa kwa sasa hawana tena kazi ya kufanya.

Wakati umoja huo ukimwangukia Rais Magufuli tayari Polisi mkoani hapa imekamata shehena ya katoni 364 ya pombe kali inayofungwa kwenye vifungashio vya plastiki ‘viroba’ iliyokuwa ikisafirishwa kutoka Jijini Mbeya kwenda mjini Sumbawanga.

Post a Comment

0 Comments