MICHAEL MTANZANIA

ONESTEPMEDIATZ

Viwavijeshi waharibu ekari 500 Chalinze




BARAZA la Madiwani wa Mji Mdogo wa Chalinze mkoani Pwani limepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali kudhibiti wadudu aina ya viwavijeshi waliovamia Wilaya ya Bagamoyo mwanzoni mwa mwezi huu na kuharibu zaidi ya ekari 500 za mashamba.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Chalinze, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Omary Zikatimu alisema hatua za haraka zilizochukuliwa na halmashauri za kusambaza dawa
za kuulia wadudu hao zimedhibiti wadudu hao katika kata zote zilizoathiriwa.

Alizitaja kata zilizovamiwa na wadudu hao ni Msoga, Pera, Kibindu, Talawanda, Mandela na Miono ambapo wadudu hao wameathiri mazao ya mahindi na mpunga.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majjid Mwanga alikiri wilaya yake kuvamiwa na viwavijeshi katika maeneo yanayolimwa mahindi kwa wingi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimuagiza Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Bagamoyo kupeleka haraka dawa iliyobakia ili kupulizia katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Ofisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Nicolaus Mgonja alisema tangu kuripotiwa kwa wadudu hao uongozi wa halmashauri uliwasiliana haraka na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kupatiwa lita 50 za awamu ya kwanza zilizosambazwa na kupuliziwa katika maeneo yote yalioathirika.

Alisema katika awamu ya pili wizara pia imeipatia halmashauri hiyo lita 50 zinazotarajiwa kusambazwa wakati wowote kuanzia sasa ili kudhibiti wadudu hao.

Post a Comment

0 Comments