MICHAEL MTANZANIA

ONESTEPMEDIATZ

KUKAMATWA KWA POMBE ZA VIROBA KWASABABISHA MFANYABIASHARA AJIUWE

Oparesheni ya wafanyabiashara wa viroba inayoendelea nchini, imesababisha Mfanyabiashara mmoja ajiue kwa kujipiga risasi kichwani.





Mfanyabiashara huyo ni mmiliki wa kampuni ya Mselia Enterprises na duka la bia za jumla, baa na nyumba za kulala wageni mjini Dodoma. Alijipiga risasi kwenye shavu la kushoto juzi, Jumanne akiwa shambani kwake Veyula, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Daktari wa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Carolyn Damian alisema alimpokea Mselia hospitalini hapo akiwa mahututi saa 7 usiku, na kumweka katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) na robo saa baadaye alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Lazaro Mambosasa alithibitisha kupewa taarifa na mtu kuhusu kusikika kwa mlio wa risasi saa 3 usiku na baadaye saa 5 aliwatuma askari na kwenda kuchunguza na ndipo walipomwona mfanyabiashara huyo, amejipiga risasi na alikufa kutokana na kutokwa na damu nyingi.
Mambosasa alisema baada ya kupewa taarifa, askari walifuatilia eneo ambalo risasi zilisikika katika shamba la mfanyabiashara huyo eneo la Veyula na walipofika, waliokota maganda matano ya risasi alizotumia kujiua.
Mfanyakazi wa mfanyabiashara huyo, Leslie Msigwa alisema ni kweli polisi walikwenda mara mbili dukani kwake Barabara ya 11, karibu na Ofisi za TFDA, na mara ya mwisho waliondoka naye akiwa kwenye gari lake prado likiendeshwa na mteja wao, Mazengo hadi waliposikia kwamba amejiua shambani kwake, Veyula Dodoma.
Msigwa alisema ni kweli kwenye stoo yake, kulikuwa na katoni 1,269 za viroba pamoja na vinywaji vingine, ambavyo huwa wanasambaza katika baa na maduka mbalimbali.
Msigwa alisema Ijumaa iliyopita, polisi walifika dukani kwake wakiwa kwenye magari mawili wakiwa na silaha, wakaingia kukagua ndani na wakaondoka na wao, wakaenda benki kuweka fedha na kulipia mzigo iliyoagizwa.
Kampeni hiyo ya kuzia pombe aina hiyo nchini, inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira ilianza Machi mosi mwaka huu, baada ya Serikali kutoa taarifa ya mwisho wa biashara hiyo tangu Mei, mwaka jana.
Mei mwaka jana, Serikali ilibainisha kuwa kuanzia kipindi hicho hadi Januari mosi mwaka huu, ungekuwa mwisho wa kuzalisha na biashara ya pombe kali inayohifadhiwa katika vifungashio hivyo (viroba).

Post a Comment

0 Comments